Saturday, December 1, 2012

Tunaamini hati haitakuwa kikwazo tena Yanga


MWISHONI mwa wiki iliyopita uongozi wa klabu ya Yanga ulisaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja mpya wa Kaunda.

Uwanja wa Kaunda ulijengwa mwaka 1973 kwa gharama ya sh3 milioni zilizopatikana kwa michango kutoka katika taasisi mbalimbali na wahisani wengine.

Huo ulikuwa ni mpango uliobuniwa na mwenyekiti wa Yanga wakati huo, Mangara Tabu Mangara alipotangaza mwaka 1970 kwamba klabu hiyo itajenga jengo lake la ghorofa mbili na uwanja kwenye makutano ya Mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam.

Ujenzi wa uwanja mpya wa Kaunda utakaotumika kwa ajili ya mechi mbalimbali za timu hiyo utaanza Juni mwakani na utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 30,000 mpaka 40,000 waliokaa.

Lengo la klabu ya Yanga kujenga uwanja huo ni kujiweka katika mazingira mazuri ya kujitegemea kiuchumi kwani uwanja huo utakuwa ni chanzo kikubwa cha mapato cha klabu hiyo.

Kwa mujibu wa uongozi wa Yanga, fedha kwa ajili ya kujenga uwanja huo watakopa benki na gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama.

Leo kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa inatarajiwa kuchukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda, ambapo uongozi wa Yanga unatarajia kulifikisha suala hilo la ujenzi huo kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo utakaofanyika Desemba 8.

Sisi tunawapongeza sana Yanga kwa kuamua kujenga uwanja wake kwa sababu itawasaidia ila suala hilo la ujenzi wa kiwanja limeonekana kama wimbo wa viongozi wa timu za Yanga na Simba kila siku kwani hata Simba pia wamesisitiza kuwa wako mbioni kujenga uwanja mkubwa wa kisasa eneo la Bunju, Dar es Salaam na kwamba utawagharimu zaidi ya Sh70 bilioni na utasimamiwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kituruki, GIDAS.

Tunasema hivyo kwa sababu mwaka 2002, aliyekuwa Rais wa Yanga Kampuni, Tarimba Abbas na baadaye mrithi wake Iman Madega (2007) wote kwa wakati tofauti waliahidi kujenga uwanja huo pamoja na jengo la ghorofa la Mtaa wa Mafia, lakini hawakufanya hivyo.

Pia, mwaka 2010 aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, aliingia makubaliano na Kampuni ya Ujenzi ya National Estate & Designing Consultancy Company (NEDCO) kwa lengo la kujenga uwanja huo, ambapo ujenzi ulitarajiwa kuanza mwezi Januari mwaka jana, lakini ujenzi haukufanyika.

Ila kwa wakati huu wa Nchunga ujenzi haukufanyika kwa sababu alitoa sababu kuwa hati za uwanja wa Kaunda hazijulikani zipo kwa nani, ambapo uongozi wa Yanga ulitoa taarifa kwamba mtu yeyote anayejua hati za uwanja wa Kaunda zipo wapi awasiline na uongozi wa klabu ya Yanga au atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi ili suala la ujenzi wa uwanja wa Kaunda lianze mara moja.

Tulishangazwa sana na taarifa hizo za uongozi wa Yanga kushindwa kufahamu zilipo hati hizo muhimu za uwanja wa Kaunda, lakini tunashangaa kusikia hivi sasa ujenzi wa uwanja wa Kaunda utaanza mwakani.

0 comments:

Post a Comment