POLISI wamewajeruhi watu watatu kwa mabomu, mmoja kati yao akiwa katika hali mbaya katika matukio mawili tofauti ya kusambaratisha mikusanyiko iliyotokea Tegeta, Dar es Salaam na Rufiji mkoani Pwani.
Aliyejeruhiwa vibaya ametambuliwa kuwa mkazi wa Tegeta, John Paul ambaye baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili.
Tukio la Tegeta lilitokea wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wananchi waliokuwa wakipinga operesheni ya kuwaondoa katika hifadhi ya barabara katika eneo hilo saa nne asubuhi baada ya wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Mwankinga wakiwa na polisi waliyolikamata gari la mkazi mmoja wa eneo hilo.
Hali hiyo ilizua ubishi na baadaye vurugu baada ya wakazi hao kutaka gari hilo lisichukuliwe na polisi.
Vurugu hizo ziliwafanya polisi kutumia nguvu kuwatawanya wakazi hao, kazi ambayo hata hivyo, haikuwa rahisi kwani nao walikuwa wakijibu kwa kuwarushia mawe na fimbo, hali iliyodumu kwa saa kadhaa na kufanya eneo hilo kugeuka uwanja wa mapambano kusababisha maduka kufungwa na mali kuharibiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Chales Kenyela alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza kuwa, kijana huyo alijeruhiwa shavuni na kitu ambacho bado hakijafahamika na kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.
Kamanda Kenyela alisema kuwa, polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na taarifa zaidi zitatolewa baadaye. Alisema awali, wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiwa na polisi, walifika eneo hilo na kuanza operesheni ya kuondoa magari.
“Walipokamata gari la mmoja wa wakazi wa eneo hilo wananchi hao walipinga na kuanza kuwafanyia vurugu polisi ambao walijibu mapigo kwa kupiga mabomu ya machozi na kuwatawanya. Kijana huyo alionekana baadaye akiwa amejeruhiwa na kupelekwa Mwananyamala,” alisema. Katibu wa Afya katika Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala alithibitisha kupokewa kwa majeruhi huyo na kudai kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa alijeruhiwa kwa bomu.
Bisakala alisema hali ya majeruhi huyo ilikuwa mbaya na uongozi wa hospitali ulilazimika kumpeleka Muhimbili kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Mmoja wa mashuhuda wa vurugu hizo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisimulia jinsi eneo hilo lilivyokuwa: “Polisi wanarusha mabomu na wananchi wanawarushia mawe, ilikuwa tafrani kubwa hapa.”
Alisema hali hiyo iliwafanya polisi wajibu kwa kupiga risasi hewani na kufyatua mabomu ya machozi hali iliyozua taharuki na baada ya watu kutawanyika, kijana huyo alionekana akiwa ameanguka chini, huku damu zikimvuja.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Eligaeshi alithibitisha kufikishwa kwa kijana huyo katika hospitali hiyo akimtaja kwa jina la John Massawe. Alisema alikuwa amejeruhiwa vibaya kichwani.
Mabomu 22 Rufiji
Wilayani Rufiji, polisi walitumia mabomu 22 ya machozi kuwatawanya wananchi wa Kijiji cha Mgomba Kati waliozingira jengo la kufua umeme wakipinga hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuondoa mashine mbili za kufua umeme bila wao kuwa na taarifa na kuzipeleka wilayani Liwale, Mkoa wa Lindi.
Mwandishi wa habari aliyekuwapo eneo la tukio saa nne asubuhi alishuhudia umati mkubwa wa watu wakiwa katika eneo hilo wakipinga kuondolewa kwa mashine hizo.
Wananchi hao walisema licha ya kuwa na umeme unaotumia gesi ya Songosongo, jenereta hizo huwasaidia wakati umeme huo wa gesi unapokosekana huku wakisema hawakushirikishwa katika uhamishwaji huo.
Askari wawili walifika katika eneo la tukio na kuwaamuru wananchi hao kuondoka katika eneo hilo bila mafanikio. Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, polisi hao walikimbia huku wananchi wakiwa na mawe wakiwafukuza. Askari mmoja aliyekuwa na bomu la machozi alidandia pikipiki na kukimbia na kumuacha mwenzake ambaye alishambuliwa vibaya kwa mawe.
Askari huyo aliyeachwa aliepuka kipigo baada ya kukimbilia katika nyumba moja ya msamaria mwema na kujificha.
0 comments:
Post a Comment