Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Bunge jana Mjini Dodoma.
Akilihutubia bunge la Tanzania, mjini
Dodoma, katikati mwa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba Tanzania
haina mpango wala fikra za kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa
ni nchi inayoamini katika umoja na maendeleo na imekuwa ikitumia gharama kubwa
kuhakikisha jumuiya hiyo inaimarika.
"Tanzania ni mwanachama mvumilivu,
mtiifu na mwaminifu na tunatimiza wajibu wetu kwa jumuiya na kuhusika
kikamilifu katika ujenzi wake." amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ametumia muda mrefu katika
hotuba hiyo kuchambua masuala mbalimbali ya msingi ya uhai wa jumuiya hiyo huku
akisema ameshangazwa na nchi za Kenya ,
Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania
na Burundi .
Amesema kuna masuala ambayo hayazifungi
nchi wanachama katika mkataba wa umoja wao, hivyo kuwa na uhuru wa ushirikiano
na nchi ndani ya jumuiya na hata nje.
"Naomba kwanza niweke wazi jambo
moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa na makubaliano ya
ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao
ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo
ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba
au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya
kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na
Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari
kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi nyingine".
Hata hivyo Rais Kikwete amesema huenda
mambo yanayoitenga Tanzania na nchi nyingine tatu za jumuiya ya Afrika
Mashariki, ni msimamo wake kuhusu kuharakisha shirikisho, masuala ya ardhi,
ajira, na uhamiaji.
Pia Rais Kikwete amesema Tanzania haina
mpango wa kujitoa kwa kuwa inaamini na ina uhakika kuwa haijafanya jambo lolote
baya dhidi ya jumuiya au nchi mwanachama yeyote wa jumuiya hiyo.
0 comments:
Post a Comment