Hapa ni Kituo cha Mizani Wilayani Mkuranga mkoani Pwani,basi likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Lindi likiwa linapima na lori la mafuta likiwa linasubiri kupima kama ilivyokutwa na mpiga picha wetu.
Hivi karibuni kumekuwa na mzozo mkubwa na mgomo wa wamiliki wa malori na mabasi katika mizani hizi kupinga kuondolewa kwa msamaha wa asilimia tano kwa mzigo unaozidi katika mzani na Serikali.Hali hii ilimfanya Waziri wa Ujenzi Bwana Magufuli kuishikia bango huku wamiliki wakisusa na kuzuia mabasi na malori yao wakidai yafuatayo: moja kutoshirikishwa na pili hiyo sheria hutumika na nchi zote jirani zinazofanya biashara na Tanzania. Kwa hali hiyo kuondolewa kwa sheria hii nchini Tanzania pekee hakuna maana.
Wakati hali hii ya mgomo ikitokea meli zimeshindwa kushusha shehena zao katika banadri yetu ya Dar es Salaam na kusababisha msongamano wa mizigo bandari na kumfanya Waziri wa Uchukuzi Dk.Mwakyembe kuwa na wakati mgumu kiutendaji.
Mwisho Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliingilia kati na kusimamisha zoezi hili na kuruhu utaratibu wa zamani kutumika mpaka hapo wadau wote wa pande mbili watakapokaa pamoja kujadili juu ya sheria hii.
Hivyo basi kwa hali hii inaonesha kabisa kiutendaji ni kama Serikali imekosa muelekeo maana inakurupuka na ukusanyaji wa kodi mbalimbali bila kushirikisha wadau kwa makini.Hii ni mara ya pili Serikali kuingia katika mgogoro na walipa kodi wake kwa mwaka huu.Ambapo awali walikuja na kodi ya tshs 1,000/= kwa mwezi kwa kila laini ya simu na kuibua mtafaruku mkubwa na wananchi hadi kufikia kusitisha kwanza kodi hiyo.
Tunaomba wataalamu wetu tuliowaweka kusimamia Serikali kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kiliingizia Taifa letu hasara kubwa na kusababisha kushuka kwa uchumi wetu. Kwa maana mgomo huu umesabisha kuchelewa kusafirishwa mizigo mikoani na nje ya nchi,huku meli zikikaa baharini foleni kusubiri kushusha shehena bandarini.Kwa maana hiyo tumepoteza mapato kwa kiasi kikubwa katika mgogoro huu.
0 comments:
Post a Comment